Karibu tena mpenzi wa Dohub, natumaini unaendelea vizuri. Nilichonacho siku ya leo ni kuhusiana na 'Agano'.
Kabla sijaanza mada hii ya leo ningepeda tufahamu kwanza utofauti na maana ya maneno haya:
- Kiapo (Oath)
- Agano (Covenant)
Kiapo ni nini?
Hii ni ahadi ya kuonesha ukweli au uaminifu, inayotamkwa mbele ya mtu, watu, au mamlaka fulani. Ni maneno yanayoweza kutamkwa kwa sababu yoyote, hata bila ukweli wa moyoni.
Mtu anaweza kuapa kwa sababu:
- Amelazimishwa (mfano: mahakamani, jeshini, mbele ya familia).
- Anafuata taratibu (ili ndoa ifungwe, ili apate kazi).
- Anataka kuonekana mzuri kwa jamii (kuwaridhisha walio mbele yake).
- Amezoea maneno, sio moyo.
- Anaongea kwa shurti, sio kwa hiari ya ndani.
Kwa hiyo:
Kiapo kinaweza kutamkwa bila moyo, ndiyo maana mara nyingi:
- Maneno ya kiapo yanaweza kuwa makubwa, lakini uhalisia wa mtu hauendani na kile alichotamka.
Hii ni tabia ya kawaida ambayo tumeizoea.
📌 Hii ndiyo sababu kiapo hakiunganishi roho ya mtu kiundani kama agano. Kwa sababu maneno yanaweza kudanganya, lakini moyo hauwezi kudanganya kwa muda mrefu.
Agano ni nini?
Ni kubaliano maalum kati ya pande mbili au zaidi, lenye masharti, ahadi, na wajibu ambao kila upande unakubali kuufuata. Ni kama mkataba, lakini mara nyingi huwa na uzito wa kiroho, kiimani, au uaminifu wa juu.
Mara nyingi maneno yanayotamkwa hapa huwa ni ya kumaanisha na endapo yatafanywa kinyume basi tutatarajia maumivu, majuto na hasara kubwa kwa sababu hunuishwa kwa roho haijalishi ni roho wa aina gani. Na hapa kwa asilimia kubwa tunapata maagano ya hisia, alama na damu.
Kuna mtu mmoja aliniuliza, "Wanandoa hula kiapo au hufanya Agano?"
Jibu langu ni kwamba:
Wanandoa huweza kufanya vyote, inategemeana na mazingira yao. Kuna wawili hukutana na kupata nafasi ya kula kiapo lakini hukosa nafasi ya kuagana. Na hawa kudumu ni mara chache sana kama nilivyokueleza tabia ya kiapo hapo mwanzo kuwa kiapo kinaweza kutamkwa bila moyo. Maneno yanaweza kuwa makubwa, lakini uhalisia wa mtu hauendani na kile alichotamka. Hapa ndoa ni ya 'Ili mradi maisha yaendelee'.
Lakini, kuna wawili hukutana na kupata nafasi ya kuagana pekee. Hawa mara nyingi hata wakivurugana, ni ngumu sana kutengana. Kuwashauri huwa ni changamoto, unaweza jikuta inakuangukia aibu kwa sababu asubuhi wanapigana, jioni wako Beach wanakula upepo mwanana.
Wa mwisho ni wale wanaoshiriki vyote, 'Kiapo' na 'Agano'. Hawa ni kumbikumbi, mwenzake akikata kona na yeye anakata kona, akisimama naye anasimama. Yaani wanafuatana kila mahali, Wanabadilishana hadi simu kuangalia comedy TikTok.
Kwanini kundi hili la mwisho limekuwa thabiti?
Kiapo humtengenezea mtu aibu(Copyright) juu ya maamzi, tabia anayoweza kufanya au kuchukua na jamii itamchukuliaje. Agano ndio kiini cha unganisho la kihisia, kimwili, na kiroho.
Kwa kifupi kabisa
- Kiapo = nguvu ya nje, taratibu, sheria, mashahidi.
- Agano = nguvu ya ndani, roho, moyo, hisia.
Kuna msemo unasema "Ukitaka kuruka, agana na nyonga"
Sasa hii tunaichukulia mfano kuwa, unapokua na mtu unamweleza na kumpa uhakika kuwa "Mimi naweza kuruka." yaani unakula kiapo. Lakini licha ya kuwa na uhakika wa kuruka unahitaji ruhusa kutoka kwa nyonga. Uagane na nyonga. Nyonga zikikataa basi kiapo cha kuruka hakina kazi tena. Lakini nyonga zikikubali muda wowote hata pasipo mueleza mtu basi unaweza kuruka.
Sasa, uzi wangu leo hii ni athari za kufanya/kuingia katika maagano bila kumulika matokeo.
Katika tafiti zangu, nimegundua athari kubwa zikitokea kutokana na maagano. Kuna baadhi ya watu wamejikuta wakijutia, kupitia changamoto mbalimbali na hii ni sababu ya maagano.
Mfano nilikutana na mzee mmoja ambaye changamoto yake ni nguvu za kiume. Hapa unaweza kujiuliza, hii imetokeaje?
Mzee huyu alinieleza kuwa kipindi alikuwa kijana, alikutana na bibie wakaweka agano kuwa hakuna mtu atamwacha mwenziye hata walithubutu kuchanja chale ili kuchanganya damu.
Anasema maisha yaliendelea vizuri wakabarikiwa watoto hadi kufikia umri wa miaka 52 muda ambao mzee huyu aliachwa na mkewe(akafariki). Kingine zaidi, siku walipokuwa hospitali waliendelea kuneneana maneno ya kuwa pamoja.
Hapo ndipo mambo ya mzee yaligeuka na mnara wa internet haukusoma H+.
Alihisi ni hali ya kawaida lakini tatizo lilikuwa zito. Alijaribu kutafuta wanawake tofauti lakini mambo hayajaenda shwari hadi sasa na kinachothibitika ni kuwa bibie aliondoka na internet kwa sababu ya agano lile.
Nje na mfano huo, kuna wengine waliagana kuwa watakufa pamoja, na ni kweli. Wakati ulipofika mme alifia kazini, mke akafia labor room siku ile ile.
Katika harakati ya kuhakikisha nafunga makala hii, nilibahatika kukutana na aunt ambaye alisema yuko na 45yrs, hajaolewa hadi sahivi. Wachumba hawaji. Kisa ni kuwa, kipindi alikuwa shule, aliweka agano na mvulana aliyekuwa naye katika uhusiano kuwa hatoolewa na mwingine zaidi yake, na hiyo ilifanyika kwa kila mmoja kuchana vipande vya nguo zao, kuvichanganya na kwenda kuvitupa mtoni. Walipohitimu tu, yule kijana akafariki. Toka yule kijana afariki baasi huyu dada hajaona kijana anaweka unyayo mbele yake.
Nikihama upande huo, kuna namna watu, familia, koo mbalimbali wamekuwa wakifanya maagano ambayo pengine yameweza kusababisha athari mbaya katika jamii zetu.
Kama nilivyosema awali kuwa agano hushirikisha roho, haijalishi ni roho ya aina gani. Yale maneno mnayokuwa mnayanena kwa makubaliano, hilo ni agano. Litafanyika hata kama mlikuwa mnajaribu kufanya.
Kwahiyo tuwe makini sana na maneno tunayotamka, matendo tunayofanya tukishirikisha roho kwa sababu yeye hututunzia kile tulichoagana.
Mpenzi wa DoHub, mimi ninaishia hapa japo nilitamani nizungumze mambo mengi katika jambo hili.
Uwe na siku njema!
Unaweza kunifuata katika mitandao ya kijamii kupitia De Opera /@deoperacc





