Asante kwa kutembelea DoHub! 😊

Ikiwa umewahi kuguswa na kile tunachokifanya, tunakukaribisha kwa upole kabisa kuunga mkono jitihada zetu iwe kwa kuchangia kiasi chochote au hata kutangaza biashara yako kupitia jukwaa hili.

KWA NINI WALOKUKATAA HUJISIKIA VIBAYA BAADA YA WEWE KUTHAMINIWA NA WENGINE?

Siraj Kingi
0

KWA NINI WALOKUKATAA HUJISIKIA VIBAYA BAADA YA WEWE KUTHAMINIWA NA WENGINE?

Karibu tena katika blog yetu ya DoHub, na ninatumaini unaendelea vizuri.

Leo nataka tuzungumzie hali ambayo ipo karibu katika kila kona ya maisha yetu, iwe kwenye mahusiano au maisha ya kawaida. Ni ile hali ambapo mtu anaonwa kama hana thamani au hahitajiki, lakini baadaye anapopata nafasi au kuthaminiwa na watu wengine, ghafla anakuwa muhimu sana machoni pa wale waliompuuza mwanzo.

Na hapo ndipo hisia za wasiwasi, majuto na hata migogoro huanza kujitokeza.

Hii inatokea vipi? (Mahusiano)

Tukianza na mahusiano, mara nyingi mtu anaweza kujaribu kuanzisha uhusiano au uchumba na mtu mwingine kwa nia ya kweli. Lakini upande wa pili ukakataa. Wakati huo, inaonekana kama hakuna kilichopotea upande wa aliyekataa. Maisha yanaendelea kama kawaida.

Lakini kinachobadilika ni pale mtu huyo huyo anapopata mtu mwingine ambaye anamthamini, anamkubali na kumpa nafasi aliyokuwa akiomba mwanzo.

Ndipo mabadiliko huanza kwa yule aliyekataa.

Anaanza kujisikia kama kuna kitu anakikosa, si kwa sababu alikihitaji sana mwanzo, bali kwa sababu sasa anaona thamani ya yule aliyemkataa kupitia macho ya mtu mwingine. Wakati mwingine huanza kuingiwa na wasiwasi, wivu, na hata hali ya kushindana kimya kimya na mtu mpya aliyeingia.

Na zaidi ya yote, kuna jambo jingine kubwa hutokea ndani yake: huanza kujiona yeye ndiye aliyekosea zaidi. Anaanza kuhisi kama yeye ndiye alikuwa na upungufu, kama alifanya uamuzi kwa haraka, na kama labda alikosa kitu muhimu sana. Hali hii humfanya mtu kupoteza kujiamini kidogo kidogo, hasa anapoona mtu aliyemkataa sasa anathaminiwa mahali pengine.

Hali hii huweza kumfanya mtu:


  • aanze kutafuta njia ya kurudi
  • au kujaribu kuingilia kile ambacho tayari kimejengwa
  • au hata kuonesha hisia ambazo hazikuwepo kabla

Lakini mara nyingi, kinachochochea haya si mapenzi mapya, bali ni mchanganyiko wa majuto, wivu, ego iliyojeruhiwa, na kuanguka kwa kujiamini.


Tukienda katika maisha ya kawaida

Hali hii haishii kwenye mahusiano tu. Inatokea pia kwenye kazi, biashara, urafiki, na hata jamii kwa ujumla.

Unaweza kuomba nafasi ya kazi ukaonekana hufai. Unaweza kutoa wazo lako likapuuzwa. Unaweza hata kutaka kushirikiana na watu fulani lakini usipewe nafasi.

Lakini muda unapopita, na ukapata nafasi sehemu nyingine, ukaanza kufanikiwa au kuthaminiwa na watu wengine, ghafla wale waliokupuuza huanza kubadilika.

Wanakutazama tofauti. Wanaanza kuona kile ambacho hawakukiona mwanzo. Na wakati mwingine, wanaanza kujutia.

Na hapa ndipo jambo muhimu hutokea ndani yao pia: mtu aliyekataa kitu mwanzo na akiona kimechukuliwa na mtu mwingine, huanza kujiona dhaifu. Huona kama yeye ndiye mwenye mapungufu, na kwamba alikosa uwezo wa kutambua thamani halisi ya kile alichokataa. Hali hii huweza kumfanya apoteze kujiamini, hasa anapoona mafanikio yako yanaendelea bila yeye.


Kwa nini watu hujisikia vibaya baada ya wewe kuthaminiwa na wengine?

Ni hali ya kawaida sana kwenye mahusiano na maisha ya kibinadamu. Mara nyingi mtu anapokataa kukupa nafasi, huwa tayari amefanya uamuzi kulingana na hisia au hali yake ya wakati huo. Lakini anapokuona baadaye ukipewa nafasi na mtu mwingine, mambo kadhaa yanaweza kutokea ndani yake:

  • Anahisi kupoteza kitu – hata kama hakukutaka mwanzo, kuona mtu mwingine akikuona wa                                                  thamani kunaweza kumfanya ajione amepoteza kitu kizuri.
  • Wivu wa asili – binadamu huwa na tabia ya kutamani kile ambacho wengine wanakithamini.
  • Majuto – anaweza kuanza kujiuliza kama alifanya uamuzi sahihi kukukataa.
  • Ego/kujithamini – wakati mwingine si mapenzi halisi, bali ni hisia ya “kwa nini sasa mtu mwingine apate kile nilichokikataa?”
  • Kupoteza kujiamini – huanza kujiona kama yeye ndiye aliyekosea, mwenye mapungufu, na  ambaye hakutambua thamani kwa wakati.

Na mara nyingi, hapa ndipo tabia tofauti huanza kuonekana. Mtu anaweza kujaribu kurudi, kuingilia maisha yako, au hata kuleta changamoto kwenye kile ulichokijenga. Si kwa sababu anakupenda zaidi sasa, bali kwa sababu hawezi kuvumilia kuona nafasi aliyokataa ikichukuliwa na mtu mwingine.

Ukweli wa maisha ni huu: sio kila anayekukataa mwanzo alikukosea, na sio kila anayekurudia baadaye anastahili nafasi ya pili.

Wakati mwingine, watu hujifunza thamani baada ya kupoteza. Lakini wewe sio lazima uwe somo la majuto ya mtu mwingine.

Endelea mbele na wale waliokuona wa maana tangu mwanzo. Linda kile ulicho nacho sasa. Na usisahau jambo moja muhimu sana:

Thamani yako haianzi pale mtu mwingine anapoiona, ilikuwepo hata kabla hajaitambua.

Ahsante sana kwa kusoma chapisho hili, nami ni De Opera | @deoperacc

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Tafadhali Usitume Barua Taka Hapa. Maoni yote yanakaguliwa na Msimamizi.
Post a Comment (0)
 
 
Tovuti yetu hutumia vidakuzi kuboresha matumizi yako. Jifunze Zaidi
Accept !