Nimefurahi kukutana nawe tena mpenzi wa Dohub, na karibu tena katika uzi huu wa leo.
Kuna watu katika maisha haya wanapigana vita ambavyo havionekani kwa macho. Unaweza ukawaona wanahangaika kila siku, wanajituma, wanaomba, wanafanya kila linalowezekana lakini mafanikio yanakuwa kama yamefungwa. Wakikaribia kuinuka, jambo fulani hutokea na kila kitu hurudi mwanzo.
Kwa mtazamo wa wengi wanaoamini mambo ya kiroho, hali hii inaweza kuhusishwa na laana, uchawi, kurogwa, kunenewa vibaya au kupandikizwa roho chafu za umasikini na kushindwa ili mtu asifanikiwe maishani.
Ndiyo maana wakati mwingine unamuahidi mtu kitu ukiwa na uhakika wa asilimia mia moja kwamba utampatia. Ghafla mambo yanabadilika. Pesa zinakwama, biashara inadorora, fursa inapotea, au kile ulichokuwa umekitegemea hakifiki. Mwishowe unajikuta unaonekana muongo, ilhali ulikuwa na nia ya dhati ya kutimiza ahadi yako.
Wapo wanaoamini kwamba wakati mwingine si wewe uliyeshindwa, bali umekutana na vita alivyowekewa yule uliyekuwa unataka kumsaidia.
Unaamua kumuinua mtu. Unampa kazi, mtaji, unamfungulia biashara au unamshika mkono kwa namna yoyote. Lakini mara tu baada ya kufanya hivyo, kila kitu kinaanza kuyumba. Miradi inasimama. Simu za michongo zinakata. Wateja wanapotea. Biashara inadoda. Kila ulilokuwa unategemea halitokei.
Kana kwamba kuna nguvu fulani inayohakikisha huna uwezo tena wa kuendelea kumsaidia.
Kwa mtazamo huo wa kiimani, wanaamini kwamba wale wanaotaka mtu huyo aendelee kubaki kwenye hali yake huangalia chanzo cha msaada/mzizi wake na kukishambulia. Yaani kwamba; "huyu si ndiye anajifanya kimbele mbele".
Lengo si lazima kukuangamiza wewe binafsi, bali kukunyima nguvu na uwezo wa kumuinua mtu wao. Wakifanikiwa kukukatisha tamaa au kukumaliza kiuchumi, msaada unasimama na yule aliyefungwa hubaki pale pale alipo.
Ndiyo maana wakati mwingine unamsikia mtu akisema, "Kila nikishirikiana na fulani napata mikosi."
Kwa mtazamo huu, si kwamba huyo mtu ndiye chanzo cha mikosi. Bali inakuwa ni kwamba amebeba vita vya kushindwa alivyowekewa, na anayejitokeza kuvunja mzunguko huo ndiye anayekutana na upinzani.
Mfano mwingine ni wa kijana anayekwenda kumchumbia binti ambaye amewekewa vizuizi vya kutoolewa. Kila kitu kilikuwa sawa. Pesa ya mahari ipo. Familia zimekubaliana. Mipango imekamilika. Ghafla misukosuko inaanza. Kijana anaishiwa fedha, anaanza kuugua, biashara yake inafungwa au matatizo yasiyoelezeka yanaibuka mpaka uchumba unavunjika.
Kwa wanaoamini mambo ya kiroho, wanaona si bahati mbaya, bali ni vita vilivyokuwa juu ya binti vimeelekezwa kwa mchumbiaji ili naye ashindwe, na binti aendelee kubaki kwenye kifungo kilekile.
Hata kwa binti pia. Kama kijana yuko kwenye vita vya kutopata kuoa, binti atajikuta kwenye changamoto za kiafya, na changamoto tu ambazo zitafanya kijana asimuoe.
Kuna msemo unaosema, "Aliyenacho huongezewa." Wengine hujiuliza kwa nini mtu aliyefanikiwa anaendelea kupata fursa zaidi, huku mwingine akihangaika bila mafanikio?
Kwa mtazamo huu wa kiimani, jibu huwa kwamba si watu wote wanabeba mizigo inayofanana. Wapo wanaoamini kuna walio huru na vikwazo hivyo, hivyo fursa zao husonga kwa urahisi. Wengine, kila hatua ya maendeleo hukutana na upinzani usioonekana.
Mara nyingi migogoro mikubwa haianzi mbali; huanzia pale ambapo tulitarajia kupata upendo na msaada. Wivu unaweza kuzaliwa ndani ya familia, ukoo, au miongoni mwa watu wa karibu. Badala ya kufurahia kuona mmoja akiinuka, wakati mwingine mafanikio yake huonekana kama tishio kwa wengine.
Wapo wanaoshindwa kuvumilia kuona mtoto wa ndugu yao akifanikiwa kuliko watoto wao. Wanahofia kwamba jamii itaanza kumtaja kama mfano wa juhudi na mafanikio, huku watoto wao wakibaki nyuma. Badala ya kumuunga mkono, huanza kumwekea mbinu wanazoamini hatafaulu.
Hali kama hiyo haipo kwenye familia pekee. Hata katika baadhi ya jamii au sehemu za kazi, wapo wasiopendezwa na maendeleo ya wengine. Wanaona mafanikio ya mtu mwingine kama kivuli kinachoanika udhaifu wao wenyewe. Kwa sababu hiyo, badala ya kushindana kwa juhudi, hujaribu kuzuia safari ya anayesonga mbele.
Pia kuna watu wanaotaka wengine waendelee kuwategemea maisha yao yote. Wanajisikia wenye nguvu pale mtu anaposhindwa kujitegemea. Wanahofia kwamba siku akisimama kwa miguu yake mwenyewe, hatakuwa tena chini ya ushawishi wao. Ndiyo maana kila dalili ya maendeleo yake huonekana kama kitu kinachopaswa kuzimwa kabla hakijakomaa. Kwahiyo wanahakikisha wanaharibu zile njia na mizizi inayoweza kumuinua.
Lakini, ni jambo la kusikitisha kuona kwamba wakati mwingine adui wa ndoto za mtu si mgeni, bali ni yule anayekula naye mezani, anayefahamu historia yake na anayejua safari yake tangu mwanzo.
Je, ulishawahi kujiuliza kwanini kuna watu ni wagumu sana kusaidia, au wanakwepa kusaidia?
Hapana, Siyo kwa sababu hana huruma, bali kwa sababu kila alipojaribu kufanya hivyo hapo awali, alijikuta naye anaingia kwenye kipindi kigumu kisichoeleweka. Ndio maana akachagua kuishi maisha hayo ya moyo mgumu.
Kiukweli, dunia imefunikwa giza ambalo hatujui yupi tumsaidie au yupi anahitaji msaada wa kweli, kwasababu imetokea mara nyingi unakutana na mtu barabarani anakufuata kukuomba msaada ambao inaweza kuwa ni pesa ya nauli au chakula, na ukimpa yeye anaenda kule ambako amepewa maelekezo ya maagano mabaya na mwisho wa siku wewe unaanza kupata magumu, kumbe ulichompa yule mtu alienda kukifanyia maagano ya giza, au umemsaidia mtu anayeteswa na mnyororo huo wa laana na bahati mbaya.
Nihitimishe kwa kusema; Maisha yanahitaji si juhudi pekee, bali pia hekima ya kuchagua watu wa kushirikiana nao, kuwa makini na mazingira yanayotuzunguka, na kutunza imani na matumaini hata pale ambapo safari inaonekana kuwa ngumu kuliko kawaida.
Kwa sababu yapo mapambano ambayo macho hayawezi kuyaona, lakini athari zake zinaweza kuonekana katika ndoto zilizokwama, ahadi zisizotimia, fursa zilizopotea na maisha yanayoonekana kurudia mzunguko uleule kila mwaka.
Nakutakia wakati mwema. Unaweza kunifuata katika mitandao ya kijamii kupitia De Opera @deoperacc, kwenye Facebook, Instagram, TikTok, na mtandao wa X.
Endelea kufuatilia Dohub(De Opera Hub).






