Karibu tena mwana DoHub. Ninanukaribisha katika makala hii ambayo nimeona niketi nikuletee ili uongeze kitu leo.
Kuna kauli moja iliyoibua mjadala mkubwa mitandaoni. Wapo walioiona kama dharau kwa majukumu ya nyumbani, na wapo walioiona kama kilio cha kutaka elimu na vipaji visitupwe. Kwa mtazamo wangu, mjadala huu umetupa nafasi ya kuzungumzia jambo kubwa zaidi kuliko kauli yenyewe.
Swali si "boksa." Swali ni: Baada ya mwanamke kusomeshwa kwa gharama kubwa na kufikia kiwango cha juu cha elimu, nani anaamua elimu yake itatumika au haitatumika?
Tuanze mwanzo.
Mtoto anapozaliwa, jukumu la kumlea, kumsomesha na kumjengea maisha ni la wazazi na jamii. Wazazi hujitolea kwa hali na mali kuhakikisha mtoto wao anapata elimu bora. Wengine huuza mali zao, hukopa fedha, hufanya kazi usiku na mchana ili kuona mtoto anafikia ndoto zake.
Lengo si kupata cheti pekee.
Elimu ni uwekezaji. Ndani yake kuna maarifa, vipaji, uwezo wa kufikiri, ubunifu na talanta ambazo zinatarajiwa kuwanufaisha mtu mwenyewe, familia yake na jamii kwa ujumla.
Lakini baada ya ndoa ndipo mjadala huanza.
Katika jamii nyingi za Kiafrika, na kwa mujibu wa baadhi ya mitazamo ya kidini na kitamaduni, mume ndiye kiongozi wa familia. Hilo lina maana kwamba maamuzi mengi ya msingi ya familia hufanyika chini ya uongozi wake.
Hapo ndipo swali gumu linaibuka.
Ikiwa mume atasema mke wake asifanye kazi, bali abaki nyumbani akiwa mama wa nyumbani, je, elimu yake yote inakuwa imepotea?
Wengine watasema ndiyo.
Wengine watasema hapana.
Lakini ukweli ni kwamba elimu haipotei eti kwa sababu mtu amekuwa mama wa nyumbani. Elimu hubaki kuwa sehemu ya utu na uwezo wa mtu. Tatizo linaanza pale ambapo uwezo, vipaji na talanta alizopewa mtu hazipewi nafasi kabisa ya kutumika.
Hapa ndipo watu wengi walitaka kueleza, lakini wakashindwa kuchagua maneno sahihi.
Kwa upande mwingine, kuna swali ambalo halipaswi kukimbiwa.
Ikiwa mwanaume ndiye anayechukua uamuzi kwamba mke wake asifanye kazi, je, amejiandaa kubeba wajibu wote unaoambatana na uamuzi huo?
Maana si haki kumzuia mke kufanya kazi huku familia ikikosa mahitaji ya msingi, watoto wakikosa mahitaji muhimu, au maisha yakitegemea kipato kisichotosha ilhali uwezo wa mke ungeweza kusaidia.
Mamlaka bila uwajibikaji ni mzigo kwa familia.
Lakini pia tutazame upande mwingine.
Je, mke anatakiwa kulazimisha kufanya kazi kwa sababu tu ana degree nne, wakati mume wake ameeleza wazi kuwa hataki?
Hili nalo si swali rahisi.
Katika ndoa, kila jambo haliamuliwi kwa kutumia cheti cha elimu, bali ndoa hujengwa kwa mazungumzo, makubaliano na kuheshimiana. Pale ambapo kila mmoja analazimisha msimamo wake, hata kama ana hoja nzuri, migogoro hunyemelea.
Ni vile wengi hufikiri jibu moja tu, kwamba 'Hapana'.
Kuna mwanaume ambaye ataona kipaji cha mke wake ni baraka kwa familia, hivyo atamsaidia akue kielimu na kikazi.
Kuna mwingine ataona mchango mkubwa wa mke wake ni kuwepo nyumbani kulea watoto na kusimamia familia.
Na kuna wengine watachagua njia ya kati, yaani mke atafanya kazi, lakini kwa namna ambayo bado familia inabaki kuwa kipaumbele.
Hakuna mfumo unaoweza kulazimishwa kwa kila familia.
Kilicho muhimu ni kwamba maamuzi hayo yafanywe kwa hekima, kwa makubaliano na kwa kuangalia maslahi ya familia yote.
Kwa maoni yangu, kosa kubwa si kuwa mama wa nyumbani.
Wala kosa si mwanamke kufanya kazi.
Kosa ni pale ambapo elimu, vipaji na uwezo wa mtu vinazimwa bila sababu za msingi, au pale ambapo mamlaka yanatumika bila kubeba wajibu unaoambatana nayo.
Elimu ya mwanamke si adui wa ndoa, na
kuwa mama wa nyumbani huku umeshika talanta/nafasi kubwa/elimu si kushindwa.
Vitu hivi viwili vinaweza kuishi pamoja kama wanandoa wanaelewana.
Mwisho wa yote, mjadala huu unapaswa kutukumbusha jambo moja muhimu. Kabla ya ndoa, watu wasizungumzie tu mapenzi. Wazungumzie pia maono ya maisha. Je, mke atafanya kazi? Je, atakuwa mama wa nyumbani? Je, wataendesha biashara pamoja? Je, watawezaje kutumia vipaji na elimu walizopewa kujenga familia yao? Waelezane mapema.
Maswali haya yakijibiwa mapema, migogoro mingi inayojitokeza baada ya ndoa inaweza kuzuilika.
Kwa sababu mwisho wa siku, ndoa si mashindano ya nani ana degree nyingi zaidi. Ndoa ni ushirikiano wa watu wawili wanaojenga maisha moja.
"Hakuna ndoa inayopaswa kuua vipaji, na hakuna kipaji kinachopaswa kuua ndoa."
Elimu ni baraka. Vipaji ni baraka. Ndoa nayo ni baraka. Hekima si kuchagua baraka moja na kuharibu nyingine, bali ni kujua namna ya kuziishi zote kwa uwiano.
Mimi naishia hapa, mpenzi wa DoHub.
Niliyekuletea makala hii ni De Opera @deoperacc. Unaweza kunifuta kwenye mitandao ya kijamii, Facebook, Instagram, TikTok, na mtandao wa X.






